Dodoma FM

Ujenzi wa eneo la machinga wazinduliwa jijini Dodoma

20 December 2021, 1:53 pm

Na; Thadey Tesha.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mh Antony Mtaka Amezindua ujenzi wa eneo la wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga lililopo Bahi Road lenye uwezo wa kuchukua wamachinga zaidi ya 3800.

Akizungumza katika uzinduzi huo mh Mtaka amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuwawezesha wafanyabiashara hao maarufu kama machinga kufanya biashara zao bila ya usumbufu wowote.

Kwa upande wake mbunge wa Dodoma mjini Mh Antony Mavunde ameishukuru serikali kwa kubuni mradi huo kwani suala la wa machinga ni moja ya mambo ambayo yalikuwa na changamoto kubwa katika jiji la Dodoma huku akibainisha kuwa kukamilka kwa eneo hilo kutafanya muonekano wa jiji la dodoma kuendelea kuwa mzuri zaidi.

Nao baadhi ya viongozi akiwemo msahiki meya wa jiji la Dodoma pamoja na mkurugenzi wa jiji wamesema mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza misongamano ya machinga katikati ya miji ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato ya jiji.

Ujenzi wa eneo hilo unatarajiwa kufanyika ndani ya siku 120 ambapo jiwe la msingi litazinduliwa machi 17 ili kumuenzi hayati rais John Pombe Magufuli na uzinduzi wa eneo hilo unatarajia kufanyika machi 19 ambapo Rais Samia atakuwa anatimiza mwaka mmoja madarakani.