Dodoma FM

Uwepo wa madawati ya jinsia katika vyuo vikuu nchini ni chachu ya kupunguza vitendo vya kikatili

13 December 2021, 2:50 pm

Na;Yussuph Hans.

Kufuatia uanzishwaji wa Madawati ya jinsia katika Vyuo Vikuu Nchini hatua hiyo imeelezwa kuwa itasaidia kwa kiasi kupunguza Rushwa ya Ngono pamoja na matukio ya ukatili wa kijinsia.

Wakizungumza na Taswira ya Habari wakazi Mkoani Dodoma wamesema kuwa uwepo wa madawati hayo huenda ikawa chachu ya kutolea taarifa vitendo hivyo.

Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia Jelda Luyangi amesema kuwa wataendelea kutoa ushirikiano kwa madawati hayo ili kutokomeza vitendo vya ukatili vyuoni vinavyoathiri mustakabali wa wanafunzi.

Naye Mwanasheria kutoka kituo Cha Sheria na Haki za Binaadamu Chemba Said Swedi amesema kuwa uanzishwaji wa madawati yanatakiwa kwenda sambamba na utoaji wa Elimu kuhusu Sheria zinazowajibisha wahusika.

Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 imeharamisha rushwa ya ngono kwa kukataza mtu yeyote mwenye mamlaka kutumia mamlaka aliyonayo katika kutekeleza majukumu yake kudai au kulazimisha upendeleo wa kingono au upendeleo mwingine wowote kama kigezo cha kutoa ajira, kupandisha cheo, kutoa haki au upendeleo wowote unaotambulika kisheria.