Dodoma FM

Tanzania yatajwa kupata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru

30 November 2021, 1:17 pm

Na; Dawati.

Katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania bara, Nchi inatajwa kupata mafanikio makubwa kupitia sekta ya maliasili, mali kale na utalii ikiwemo kukuza na kuimarisha shughuli za utalii Nchini.

Naibu Waziri wa maliasili na utalii Mh. Merry Masanja ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma wakati akilezea mafanikio, changamoto na mikakati ya Wizara hiyo kuelekea miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara.

Amesema miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara Serikali imefanikiwa kuimarisha utalii Nchini na kuongeza idadi ya watalii kutoka 9847 mwaka 1960 hadi kufikia watalii 1,527,230 mwaka 2019.

Amesema kumekuwepo na ongezeko la mapato yatokanayo na watalii kutoka dola za kimarekani milioni 259.44 mwaka 1995 hadi kufikia dola za kimarekani Bilioni 2.6 mwaka 2019.

Naibu Waziri Merry amesema Wizara imeendelea kuhamasisha vivutio vya utalii na kupata umaarufu mkubwa kimataifa ikiwemo hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuwa hifadhi bora Barani Afrika kwa miaka mitatu mfululizo.

Amewataka watanzania kuipenda Nchi kwa kuisemea vizuri katika mataifa mengine pamoja na kuanzisha utamaduni wa kujiajili kupitia sekta ya utalii.