Dodoma FM

Mchango wa sekta ya madini waongezeka na kufikia asilimia 7.7

5 November 2021, 12:59 pm

Na;Mindi Joeph .

Waziri wa Madini Dotto Biteko amesema Mchango wa sekta ya madini umeongezeka na kufikia asilimia 7.7 ya pato la taifa katika robo ya pili ya mwaka 2021 huku ukitarajiwa kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari juu ya mafanikio na maendeleo ya Sekta ya madini kabla na baada ya uhuru kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa tanzania bara amesema Serikali imefanya jitihada kubwa za kuhakikisha watazania wananufaika na rasilimali za madini na mapinduzi makubwa yamefanyika.

Ameongeza kuwa Katika mwaka 2020 sekta ya madini ilichangia asilimia 6.7 kwenye pato la taifa na hivi karibuni mchango wa sekta ya madini umeongezeka hadi kufikia asilimia 7.7 katika robo ya pili ya mwaka 2021 aprili hadi june.

Katika hatua nyingine amesema ushiriki wa watanzania katika uchumi wa madini umeongezeka tofauti na miaka iliyopita kabla ya kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ya madini mwaka 2017.

Tanzania imeendelea kufungua shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kwani hadi kufikia septemba 2021 leseni hai ambazo zimeshatolewa za utafutaji wa madini ni 1,044 leseni 15 za uchimbaji mkubwa leseni 161 za uchimbaji wa kati leseni 3,4000 za uchimbaji mdogo na leseni 1561 za biashara ya madini.