Dodoma FM

Watu wenye ulemavu wameshauriwa kuacha kujitenga na jamii ili kuepuka ukatili

1 November 2021, 12:15 pm

Na; Mariam Matundu.

Watu wenye ulemavu wameshauriwa kuacha kujitenga na jamii ikiwa ni mbinu moja wapo ya kuepuka ukatili dhidi yao ikiwa ni pamoja na kutengwa na kuitwa majina dhalilishi.

Hayo yamesemwa na mdau wa masuala ya watu wenye ulemavu Enock Mbawa wakati akizungumza na taswira ya habari na kuongeza kuwa jamii inatakiwa kuelewa kuwa mtu mwenye ulemavu ni mtu sawa na watu wengine isipokuwa tofauti ya kimaumbile .

Stephen Katembo ni Mtu asiyeona amesema kuwa kitendo cha kumfanyia ukatili mtu mwenye ulemavu hususani kumnyanyapa inasababisha mtu huyo kupoteza amani na kuanza kuwaza mambo mengi.

Kwa upande wake Mwanaharakati wa masuala ya watu wenye ulemavu Bi Witness akizungumzia namna wanavyowajibika kusaidia jamii kukomesha ukatili kwa watu wenye ulemavu amesema kuwa njia ambazo wamekuwa wakizitumia ni kuripoti matukio ya ukatili kwenye vyombo vya dola na serikali ya mtaa

Pamoja na hayo jamii inapaswa kuendelea kuweka juhudi za kukinga, kuzuia, kuripoti na kukabili ongezeko la hatari la unyanyasaji kwa watu wenye ulemavu huku pia wakiwajumuisha na kutowabagua watu wenye ulemavu.