Dodoma FM

Mbegu ya Alizeti kuuzwa kilo moja kwa shilingi 3500/=

25 October 2021, 11:36 am

Na; Mariam Kasawa

Serikali imesema kilo moja ya mbegu bora ya alizeti itauzwa kwa Sh.3,500 kwa wakulima ili kuinua kilimo hicho na kukabiliana na tatizo la upungufu wa mafuta ya kula nchini.

Waziri wa Kilimo, Pro.Adolf Mkenda, aliyasema hayo kwenye uzinduzi wa mpango wa usambazaji wa mbegu za alizeti kwa wakulima ambapo Sh. bilioni 2.2 zimepangwa kutumika kununua na kugawa mbegu hiyo kwa wakulima.

Alisema lengo ni kuokoa zaidi ya Sh. bilioni 500 ambazo hutumika kwa mwaka kuagiza mafuta hayo nje ya nchi.
Alibainisha kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha tatizo la uhaba wa mbegu linatatuliwa miaka michache ijayo.
Alifafanua kuwa wameteua mikoa mitatu ambayo italima alizeti chini ya usimamizi mzuri ili kuzalisha mbegu hizo kwa wingi.

Kadhalika, alisema wameongeza fedha za mafunzo kwa maofisa ugani na mabwana shamba ili kuwapa maelekezo mazuri wakulima.

Pia alisema wataendelea kuyapa kipaumbele mazao ya pamba, michikichi, karanga na mengine ili kumaliza uhaba wa mafuta nchini.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa, Dk. Fatma Mganga, alisema ekari 800,000 zimetengwa kwa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kupanda mbegu hizo.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Mkunda, alimhakikishia Waziri wa Kilimo kuwa mbegu hizo zitatunzwa vizuri na wakulima wote watazipata.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Dk. Sophia Kashenge, alisema kama taasisi inaendelea kufuata maelekezo ya Wizara ya Kilimo na kuhakikisha tatizo la mbegu linakwisha.