Dodoma FM

Wananchi waonyesha muitikio mdogo katika kujitokeza kupima Afya ya macho

22 October 2021, 12:15 pm

Na;Yussuph Hans.

Licha ya Serikali kuhakikisha Huduma ya upimaji Macho inapatikana katika vituo mbalimbali vya afya nchini, imeelezwa kuwa kasi ya kujitokeza kupima Afya ya Macho kwa Wananchi bado ndogo.

Wakizungumza na Taswira ya Habari baadhi ya Wakazi jijini hapa, wamesema katika kipindi chote hawakuwahi kupima Afya ya Macho kwa kile walichodai kuhofia gharama za Hospitali.

Hapo jana wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Afya Macho Duniani iliyoenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Penda Macho Yako Kila Mmoja Anahusika Nenda Kapime Sasa” Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi yenye wagonjwa wengi wasioona.

Ameongeza kuwa Pamoja na ukuaji wa huduma za utambuzi wa Magonjwa ya Afya Macho Nchini, bado kuna watu wengi hawajafikiwa na huduma hiyo kutokana na ongezeko la idadi ya wagonjwa kila Siku.

Magonjwa mbalimbali ya Macho yanaweza kutibiwa na kupona endapo yatabainika mapema huku serikali ikiendelea kusisitiza jamii kujenga desturi ya kupima afya zao mara kwa mara.