Dodoma FM

Serikali ya Tanzania yaendelea kuimarisha ushirikiano na nchi jirani ikiwemo katika sekta ya kilimo

21 October 2021, 1:49 pm

Na; Selemani Kodima.

Serikali ya Tanzania imeendelea na juhudi zake za kuimarisha ushirikiano na nchi jirani ikiwemo Burundi ambapo pamoja na mambo mengine imekusudia kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo.

Kufuatia ushirikiano huo Waziri wa kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda amefanya ziara ya kikazi nchini Burundi ambapo aliwasili Tarehe 18 Octoba 2021 na kuanza ziara ya siku mbili tarehe 19-20 Octoba 2021.

Pamoja na mambo mengine katika ziara hiyo Waziri Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide ambapo kwa kauli moja wamekubaliana kuendeleza ushirikiano maradufu.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Ngozi na Kayanza alipotembelea kujionea mashamba ya Kilimo cha mahindi (Block Farming) pamoja na kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Nchini Burundi ya Isabu, Waziri Mkenda amesema kuwa lengo la ziara yake katika maeneo hayo ilikuwa ni kujionea hali ya ubora wa mazao ya wakulima yanayotumia mbolea ya FOMI.

Waziri Mkenda amemuhakikishia mwenyeji wake ambaye ni Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide kuwa atampatia mualiko ili aweze kutembelea Tanzania kwa ajili ya kujifunza kuhusu kilimo cha mazao mbalimbali na kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Amesema kuwa viongozi wakuu wa nchi zote mbili Tanzania na Burundi wamekuwa wakijenga uhusiano mzuri wa Kidiplomasia na kisiasa kwani wananchi wameendelea kufanya biashara za mazao bila vikwazo hususani mazao ya mahindi, mchele na Parachichi.