Dodoma FM

Waziri wa kilimo Prof. Adolf Mkenda atembelea kiwanda cha mbolea cha FOMI nchini Burundi

20 October 2021, 12:08 pm

Na; Selemani Kodima.

Waziri wa Kilimo Mh. Prof Adolf Mkenda ameendelea na Ziara yake nchini Burundia ambapo amefanya mazungumzo na Menejimenti ya kiwanda cha Mbolea cha FOMI ambacho kupitia kampuni yake ya ITRACOM imeanza ujenzi wa kiwanda cha mbolea Jijini Dodoma nchini Tanzania.

Katika ziara hiyo Waziri Mkenda pamoja na wataalamu mbalimbali aliombatana nao amekagua kiwanda cha FOMI na kuona kinavyofanya kazi ikiwa ni lengo la kuona uwezekano wa kiwanda hicho kama kinaweza kuuza mbolea yake Tanzania kwa bei nafuu kwa wakulima na kupatikana kwa wingi na kwa wakati.

Prof Mkenda amesema kuwa kiwanda hicho nchini Burundi kinazalisha Tani kati ya 120,000 mpaka Tani 150,000 kwa mwaka kulingana na soko la mbolea huku kikiwa kimeanza ujenzi wa kiwanda cha kisasa Jijini Dodoma nchini Tanzania ambapo kitapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha Tani 600,000 za mbolea

Amesema kuwa wakati serikali inaendelea na mkakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea Tanzania vilevile inaendelea na mkakati wa kuhakikisha kuwa inatafuta mbolea inayoweza kupatikana kwa wakati na kuwafikia wakulima kwa bei nafuu.

Waziri Mkenda amemuhakikishia Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Bw Ntirampeba Simon kuwa serikali ya Tanzania itakuwa bega kwa bega kuhakikisha kuwa ujenzi wa kiwanda hicho unakamilika kwa wakati uliokusudiwa.

Kwa upande wake Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide amesema kuwa mazungumzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani yameongeza wigo mpana Zaidi kwa kubadilishana mawazo katika sekta ya kilimo.