Dodoma FM

Wanawake ni muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote Duniani

15 October 2021, 11:36 am

Na ; Selemani Kodima.

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameonesha kuwa wanawake ni muhimu katika maendeleo ya taifa lolote kulingana na asili ya majukumu yao wanayoyafanya hasa katika malezi kwa mtoto.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima mara baada ya kushiriki kwenye Kongamano la tatu la Wanawake lililofunguliwa na Rais huyo na kuhudhuriwa viongozi wa mataifa mbalimbali.

Dkt. Gwajima amesema kuwa Rais huyo amebainisha kwamba ni namna gani wanawake ni muhimu katika hatua za awali za malezi na makuzi ya mtoto ambapo mambo mengi ya msingi ambayo mtoto anapaswa kupatiwa katika msingi wa makuzi yake mwanamke anahusika moja kwa moja kwani muda mwingi anakuwa na mtoto katika malezi yake.

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa wanawake ndio wanaoleta Taifa kuwa na sura fulani na tabia nyingi wanazorithi watoto wetu wakiwa wadogo zinabaki katika kumbukumbu zao na ndizo zinazojenga taifa mbele ya safari.

Hata hivyo Dkt. Gwajima ameahidi kutokana na Kongamano hilo Serikali ya Tanzania itajipanga kuwa na kongamano la Wanawake kupitia Majukuwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ambayo yapo kwenye ngazi za halmashauri hadi Mikoa ili kuweza kujiandaa kwa miaka inayokuja kuwasilisha yatokanayo na kongamano hilo.

Kwa upande wa utalii Waziri huyo aliwathibitishia Urusi kuwa Tanzania inapokea idadi kubwa ya watalii kutoka mataifa mbalimbani na kwamba idadi ya watalii kuanzia Mwezi Agosti 2020 hadi Februari, 2021 zaidi ya watalii laki moja (100,000) waliweza kuingia Tanzania na waliondoka wakiwa salama.