Dodoma FM

Wakulima jijini Dodoma waahidi kulipa asilimia 5% ya wastani wa mavuno kwa mwaka

13 October 2021, 1:50 pm

Na;Mindi Joseph .

Wakulima Jijini Dodoma wameahidi kutekeleza ulipaji ada ya asilimia tano 5% ya wastani wa mavuno kwa msimu wa mwaka kwa hekari katika kuendelea kukuza kilimo cha umwagiliaji Nchini.

Taswira ya habari imezungumza na wakulima Wilayani bahi ambapo wamebainisha kuwa katika kutambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji wanafanya jitihada pindi wanapovuna kuhakikisha wanalipia ada hiyo.

Akizungumza na baadhi ya wananchi kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Mohamed Mcheni Afisa Kilimo Mwandamizi amesema kuwa, taratibu zote za ukusanyaji wa ada zimekamilika na kutangazwa katika gazeti la serikali Kwa mwaka huu wa fedha na miaka inayoendelea wataendelea kukusanya asilimia tano.

Aidha Bw. Mcheni amesema kuwa Asilimia tano ni sawa na wastani wa gunia moja kwa hekari kwa zao la mpunga na anasema chama cha wakulima katika skimu za kilimo cha umwagiliaji zinatakiwa kulipa ada ya usajili kiasi cha shilingi laki moja na elfu sabini na tano.

Ushiriki wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika Maonesho hayo kuelekea maadhimisho ya kilele cha siku ya Chakula Duniani yenye kauli mbiu inayosema “Zingatia Uzalishaji na Mazingira Endelevu kwa lishe na Maisha Bora” yanayofanyika Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro inatoa fursa kwa tume hiyo kutoa elimu Zaidi kwa wakulima.