Dodoma FM

Athali za mabadiliko ya tabia nchi zachangia kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari

11 October 2021, 11:59 am

Na; Mindi Joseph.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo amesema athari za mabadiliko ya tabia Nchi zimechangia kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari na kusababisha kisiwa cha maziwe Wilayani pangani na kisiwa cha fungu la nyani Wilaya ya rufiji kumezwa na maji ya bahari.

Waziri Jafo ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akizungumzia msimamo wa Tanzania kuelekea kwenye majadiliano ya mkutano wa 26 wa Nchi wanachama wa mkataba wa umoja wa mataifa unaotarajia kutafanyika jijini Glasgow Nchini Scotland.

Amesema mkutano huo utaanza Octoba 31 mpaka 12 Novemba na kuhudhuriwa na takrabani wanachama 3000 kutoka Nchi mbalimbali Duniani ambapo lengo la mkataba huo ni kuhakikisha mlundikano wa gesi joto angani unaosababishwa na shughuli za binadamu unakuwa katika kiwango ambacho hakileti madhara kwa binadamu.

Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi miradi mbalimbali imetekelezwa ikiwemo kujenga kuta za bahari kwa ajili ya kuzuia mmomonyoko wa fukwe na kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 Serikali imetumia takribani bilioni 362.

Taswira ya habari imezungumza na Mdau wa mazingira Henry Kazula kutoka taasisi ya Jielimishe kwanza ambae amesema wanashirikiana kikamilifu na jamii katika kuhakikisha wanakabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Suala la upunguzaji wa gesijoto kwenye uso wa Dunia halina budi kufanyika ili ongezeko la joto liwe chini ya nyuzi  2°C na juhudi za ziada zinahitajika ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.