Dodoma FM

Tume ya Taifa ya umwagiliaji yatarajia kutoa elimu kwa wakulima

7 October 2021, 11:59 am

Na;Mindi Joseph.

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inatarajia kuanza kampeni mwezi huu ya kutoa elimu kwa wakulima kuchangia ada kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji pamoja na kutatua changamoto ya skimu mbalimbali Nchini.

Hayo yanajiri wakati Tanzania inakadiriwa kuwa na skimu 2773 za umwagiliaji huku skimu nyingi kati ya hizo hazifanyi kazi kutokana na changamoto ya kukosa matengenezo na kuchangia uzalishaji wake kutofikia kiwango kilichotarajiwa.

Akizungumza na Taswira ya habari Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Daudi Kaali amesema Mwaka jana Serikali ilianzisha mfuko wa umwagiliaji ili kugharamia matunzo na uendeshaji wa skimu hapa Nchini.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi uendeshaji Bw. Enterbet Nyoni amesema Bunge lilipitisha asilimia 5 kwa ajili huduma ya umwagiliaji kwa wakulima kwa wastani wa pato lake ambapo asilimia tano itahusisha asilimia 75% kubakia katika skimu husika na asilimia 25% itakwenda katika mfuko wa maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji.

Katika kutekeleza agizo la Serikali kwa wakulima wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji kuchangia asilimia tano Tume ya taifa ya Umwagiliaji imekamilisha Miongozo kanuni na taratibu za ukusanyaji wa tozo na hivi karibuni itaanza kampeni ya kutoa elimu kwa wakulima katika Mikoa sita ambayo ni Arusha, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Mbeya na Morogoro.