Dodoma FM

Mfumo dume unavyo waathiri wanawake katika uzalishaji wa mazao wilayani Bahi

1 October 2021, 12:20 pm

Mwandishi Mhindi Joseph.

Mfumo Dume ni matokeo ya dhana za kurithi, imani za kidini, mila na tamaduni ambazo zinamkandamiza mwanamke katika uzalishaji wa mazao.

Mchango wa wanawake katika uhakika wa upatikanaji wa chakula na lishe ni mkubwa kwani asilimia 72 ya wanawake ndio mhimili mkuu wa uzalishaji wa mazao ya chakula katika kaya.

Kilimo ni Sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania kwa kuwa ni chanzo kikuu cha chakula, ajira, fedha za kigeni na malighafi zinazotumika viwandani na uzalishaji wa chakula unaweza kuongezeka hadi asilimia 10 na hivyo kupunguza umaskini hadi asilimia 13.

Takribani asilimia 60 ya wanawake ndio nguvukazi inayotumika kwenye kilimo cha kaya, wakiwajibika na upanzi wa mboga, uhifadhi wa mavuno na ufugaji wa Wanyama kama vile mbuzi na kondoo na Wanawake pia wanawajibika kwa lishe ya familia kupitia jukumu lao la kuandaa mlo wa familia.

Mtakwimu Mkuu wa Serikal Dkt. Albina Chuwa anasema Matokeo ya Sensa ya kilimo ya mwaka 2019/20 yanaonesha kuwa kati ya kaya 12,007,839 zilizopo Tanzania kaya 7,837,405 sawa na asilimia 65.3) zinajihusisha na shuguli za kilimo Kati ya hizo, kaya 5,088,135 sawa na asilimia 64.9 zinajihusisha na kilimo cha mazao tu.

Kaya zinazojihusisha na shughuli za “mazao zimeongezeka kutoka milioni 3.5 mwaka 2007/08 na kufikia milioni 5.1 mwaka 2019/20 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 45.7 kwa Mujibu wa Mtakwimu Mkuu wa Serikal Dkt. Albina Chuwa.

Mfumo dume unaendelea kuonekeana katika uzalishaji wa mazao ya chakula pamoja na uuzaji wa mazao kwa wanawake hivyo jitihada zinahitajika na changamoto hii lazima lishughulikiwe haraka ili kutokomeza athari zinazojitokeza kwani baadhi ya kaya zinakabiliwa na Njaa.

Nimekuja kijijini Kigwe kijiji ambacho kimejikita zaidi katika kilimo cha zao la karanga.
Karanga ni zao linalolimwa maeneo mengi nchini Tanzania na hutumiwa kwa matumizi mbalimbali kama chakula na kutengeneza mafuta.

Katika kijiji cha kigwe wakulima huzalisha zao la Karanga ambalo hustawi maeneo yenye hali ya hewa yenye baridi lakini pia na kiangazi kirefu chenye joto na hustahimili ukame kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkoani Dodoma kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2020 unaonesha kuwa kuanzia Januari hadi Disemba kwa mwaka 2020 wanawake 56 waliripoti Dawati la Jinsia kutokana na kukabiliwa na Mfumo Dume Kwenye uzalishaji wa chakula na kuchangia ukatili wa kiuchumi.kwa mujibu wa Takwimu za Dawati la jinsia Wilaya ya bahi.

Katika wanawake 10 niliozungumza nao wanawake 7 wameathirika na mfumo dume katika uzalishaji wa mazao ya chakula kwenye familia zao.

Prisca Malima ni mkulima Katika kijiji cha kigwe wilayani bahi ana simulia jinsi mfumo dume ulivyomuathiri katika uzalishaji wa mazao na kukata tamaa kulima kwani alijitoa na mwisho wa siku hakupata haki yake.
“Mimi nilikataa tamaa kabisa kulima kwani kwenye maamuzi baada ya kuvuna sikupewa hata nafasi ya kushiriki katika kuuza mazao ambayo tulilima pamoja na mume wangu alikuwa anauza na hanishiriki hali ambayo ilichangia wakati mwingine familia yangu kukosa chakula cha watoto wangu”
“Watoto wangu walikosa chakula na nilihangaika sana ila hadi sasa bado nawaona wanawake wengine wanateseka hivyo nguvu kubwa inahitajika kuondoa mfumo dume katika uzalishaji wa mazao pamoja na kuuza kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”

Situmai ally self ni mama wa familia na Mkulima anasema Mfume dume unadumaza kilimo kwani wanawamke hawashirikishwi chochote baada ya kuvuna mazao.
“Thamani kama mwanamke Sikupewa kwani tulilima pamoja mazao ya chakula na tukavuna mwanaume wangu akauza mazao pekee yake pasipo kunishirikisha na pesa alizopata akaenda kunywa pombe pesa zote za mazao aliyouza akaniacha nahangaika na watoto wangu chakula ndani hakuna”
“ Niliteseka sana na watoto wakati mwingine tunashinda njaa kwani yeye alikuwa anarudi nyumbani amelewa na hajali kama chakula hakuna ndani”

John athanasi kalua ni Mkulima wa kijiji cha kigwe na Baba wa Familia anakiri wanaume wengi kuendekeza mfumo dume kwani anasema takribani asilimia 80 ya wanaume bado wanamfume dume katika kijiji cha kigwe kwani wanaume wanawimiliki wanawake na watoto.

“Sisi wanaume bado tuna desturi ya kumiliki mali zote na kaya nyingi bado zinaishi hiyo kwani maamuzi mengi wanafanya wao iwe kwenye kuuza mazao waliyovuna licha ya kwamba wanawake wanaachiwa kulima kwa kiasa kikubwa wao ndio wanaenda shambani kwani wanaume wengi wanaenda kwenye vibarua”
Afisa mtendaji kijiji cha Kigwe Lucas Majuto anasema uzalishaji wa mazao unapungua utokana na mfumo dume kijiji cha kigwe kinalima sana zao la karanga na wanaume ndio wavunaji wa zao hilo na mfumo dume bado unakikabili kijiji hicho.

“Wanaume ndio wamiliki wa chakula cha kaya kwani wanajichukulia mamlaka ya kuuza chakula kilichozalishwa na familia na ndoa nyingi zinayumba na zingine kuvunjika na kurudisha nyuma maendeleo ya kaya hivyo ni wakati wa wananume kubadilika na kushirkiana na wanawake katika maamuzi ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na kukuza kipato”
“Wanawake ndio nguzo ya kaya kwani wanalima lakini chakula kikishavunwa mwanaume anauza bila kumshirika mke wake”

Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Dodoma Bi.Honoratha Rwegasira amesema kuwa katika Mkoa wa Dodoma bado kuna mfumo dume hususani vijijini katika kilimo na serikali inaendelea kufanya jitihada ya kutoa elimu kutatua changamoto hiyo kwani inarudisha nyuma uzalishaji wa kaya.

“Mkoa wa Dodoma Bado kuna mfumo dume katika kilimo na elimu tunaendelea kuitoa ili kuimarisha maendeleo ya kaya tunawashauri Baba na Mama kukaa pamoja na kushirikishana katika kuuza mazao waliyolima pamoja ili kuondoa migogoro kwa familia inayojitokeza baada ya mazao kuvuna tunazihimiza familia kungawa au kuuza mazao waliyolima kwa pamoja licha ya uwepo wa changamoto ya kubadilisha wanaume wengi wanaoendekeza mfumo dume”

Afisa jinsia kutoka shirika la Farm Africa shirika linalolenga kukuza zao la mtama kwa Wakulima na kuongeza uzalishaji wa chakula wenye ufanisi Bi Helena Lawi anasema bado kuna changamoto katika ushirikishwaji wa maamuzi katika kilimo kwa wananwake.
“Zaidi ya asilimia 72 ya wanawake ndio wanashiriki Zaidi katika kilimo kuandaa mashamba pamoja na kuvuna laki lipokuja suala la soko mfume dume unaaza kwani mwanaume anakuwa anaona ni haki yake yeye kwenda sokoni kuuza mazao na akishauza anatokomea na hela na zikiisha anarudi nyumbani akiwa hana kitu”
“Tunatoa elimu Zaidi ya wanaume kushirikiana na wanawake pamoja na familia katika maamuzi na mabadiliko yameanza kujitokeza japo itachukua muda kutatua changamoto hii”

Afisa kilimo Halimashauri ya wilaya ya Bahi Dominica Sambangi anasema wanahimiza wakulima kulima kwa kutumia mbinu bora za kilimo ili wakulima wawe na ziada ya chakula na kuondokana na njaa na wanawahimiza wakulima kulima mazao ya kutosha ili kupunguza njaa na kuinua uchumi kwani Mkoa wa Dodoma umewahi kukabiliwa na njaa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na wakulima walilima pasipo kuzingatia kanuni bora za kilimo”

“Mfumo dume katika wilaya ya bahi upo kwa kiasi kikubwa kwani wanawake wanalima lakini wakati wa kuuza wanawake wanatengwa na hata bei za kuuzia mazao wanawake wengi hawajui”
“Mwanamke anaathirika kutokana na kutoshirikishwa na mume wake wakati wa kuuza mazao na inapunguza kiwango cha wanawake kushiriki Zaidi kilimo na kushusha uchumi wa familia”

“Tumegundua changamoto hii ni kubwa hivyo nguvu na tunatakiwa kufanya jitihada Zaidi ya kutoa elimu kwa wakulima wanawake pamoja na wanaume kuwepo kwa usawa na kushirikiana kwa pamoja kwani kaya zinazoshirikiana katika uzalishaji na uuzaji wa mazao zinamaendeleo Zaidi”

“Tunawashauri wanaume kushirikiana na wanawake kwa asilimia 50 kwa 50 katika mambo yote ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwani hii ndio nguzo ya kukuza uchumi wao na kuondokana na mfumo dume pamoja na kushirikiana katika kila Nyanja ya uzalishaji kwani itaongeza tija katika kilimo