Dodoma FM

Wakazi wa kijiji cha Iyumbwi wakumbwa na sintofahamu ujenzi wa vyumba vya madarasa.

24 September 2021, 9:24 am

Na; Mariam Matundu .

Katika kuendelea kutatua changamoto za miundombinu ya elimu wakazi wa Kijiji cha Iyumbwi Kata Ya Nghumbi Wilayani Kongwa wanaendela na ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya msingi Iyumbwi kwa nguvu zao .
Katika ujenzi huo uliochukua takribani miaka miwili bila kukamilika umeleta sintofahamu kwa wakazi wa Kijiji hicho kwa kuwa wamekuwa wakitoa michango mara kwa mara .

Akizungumza na taswira ya habari mmoja wa wakazi katika Kijiji hicho amesema wanashindwa kuelewa ni nini kinakwamisha kukamilika kwa madarasa hayo kwa kuwa wamekuwa wakitoa michango kila wakati.

Bw. Michael Eliasi mwenyekiti wa Kijiji hicho amesema kuwa sababu ya kuchelewa kukamilika ni mafundi ambao walikuwa wanajenga sehemu nyingine lakini hata hivyo wanatarajia kukamilisha ujenzi huo mwishoni mwa mwezi huu.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Nghumbi Sima Mude amesema kupitia michango ya wananchi wanajenga vyumba vitatu vya madarasa hadi katika ngazi ya kuezeka na halmashauri imeahidi kutoa mabati na kukamilisha ujenzi wote.

Wananchi wanawajibu katika kuchangia maendeleo yoyote katika eneo lao ikiwa ni pamoja na suala la elimu ambapo serikali kupitia halmashari zimekuwa zikimalizia ujenzi walioanzisha wananchi.