Dodoma FM

Dodoma waidhimisha siku ya amani duniani kwa kudumisha amani mitaani

21 September 2021, 12:20 pm

Na; Shani Nicolous.

Kufuatia maadhimisho ya siku ya amani Duniani mwenyekiti wa wenyeviti wote jijini Dodoma Matwiga Kiyatya amesema wajibu wao ni kuhakikisha mitaa yote jijini inakuwa katika hali ya amani.

Akizungumza na Taswira ya habari kupitia kipindi cha Dodoma live mwenyekiti huyo amesema kuwa wamejipanga vikali kupambana na vitendo vya uvunjivu wa amani katika mitaa kwa kushirikiana na wananchi wa mitaa hiyo.

Amesema kuwa jukumu la kwanza la Wenyeviti wa mitaa ni kuhakikisha amani inakuwepo kwa kushirikiana na Watendaji wa mitaa na kata kwani wao wakidorora katika kuwajibika mambo hayawezi kwenda ipasavyo.

Kwa upande wake Askofu Yohana Masinga amesema kuwa kama viongozi wa dini wanahakikisha kila kinachofanyika kinahamasisha amani hata kuandaa maombi maalumu ya kuiombea nchi idumu katika amani.

Dodoma fm imezungumza na baadhi ya wananchi jijini hapa na kusema kuwa wanaipongeza nchi ya Tanzania kwa kuwa na amani hivyo serikali iimarishe ulizi hasa katika mipaka ya Tanzania na kuliongezea nguvu jeshi kwaajili ya ulinzi.

Kila ifikiapo septemba ishirini na moja kila mwaka dunia huadhimisha siku ya amani duniani na kaulimbiu ya maadhimisho ya amani mwaka huu inasema”kujikwamua vyema zaidi kwa ulimwengu kwa maendeleo endelevu.