Dodoma FM

Jamii imetakiwa kuacha kuwafanyisha kazi za ndani watoto wenye umri chini ya miaka 18

16 September 2021, 12:59 pm

Na; Benard Filbert.

Jamii imetakiwa kuacha kuwachukua watoto chini ya miaka 18 kufanya kazi za ndani kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria za Nchi ya Tanzania.

Hayo yameelezwa na afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Dodoma Bi. Honoratha Rwegasira wakati akizungumza na taswira ya habari kuhusu kuzuia ukatili wa kijinsia hususani kwa mabinti wa kazi za ndani.

Bi. Honoratha amesema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiwachukua watoto wadogo ambao hawajafikisha umri wa miaka 18 kufanya kazi za ndani katika maeneo ya mijini kitu ambacho ni kinyume na sheria za Nchi.

Aidha ameongeza kuwa pale wanapobaini ukatili wa kijinsia kwa mabinti wa kazi wamekuwa wakiwaunganisha na dawati la jinsia ili kufuatilia kwa ukaribu suala hilo.

Baadhi ya wananchi wakizungumza na Dodoma FM wamesema kuwa sio sawa kuwachukua watoto chini ya miaka 18 na kuwaweka kuwa wafanyakazi wa ndani kwani ni kuwakosesha haki zao za msingi ikiwemo kuendelea na masomo.