Dodoma FM

Uelimishaji na uhamasishaji wa sensa utasaidia kuongoza uelewa kwa jamii

15 September 2021, 2:48 pm

Na ;Shani Nicolous .


Siku moja baada ya uzinduzi wa mpango wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 uliofanyika jana baadhi ya wananchi wameeleza kuwa mpango huo utasaidia kuongeza uelewa katika jamii juu ya umuhimu wa sensa.

Wakizungumza na Taswira ya habari wananchi hao wamesema wapo baadhi ya watu wanaotambua maana ya sensa hivyo ni muhimu kwa serikali kuwatumia viongozi katika ngazi zote na taasisi binafsi ili kutoa elimu hiyo.

Wamesema kuwa sensa ni muhimu katika Taifa lolote linalopenda maendeleo kwani inasaidia viongozi kupanga bajeti sahihi kwa ajili ya wananchi waliopo na hata kuongeza mapato kwa ukusanyaji wa kodi sahihi kwa wananchi na makazi.

Taswira ya habari kupitia kipindi cha Dodoma live imemtafuta Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Mh. Jabil Shikimweli ambaye amesema kuwa wameunda kamati mbalimbali ambazo zitasaidia kutoa elimu kwa njia mbalimbali kwa jamii ili kuendelea kukuza uelewa juu ya sensa.

Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kujitoa kwa ajili ya zoezi hilo muhimu la kitaifa pia vongozi wa dini, vyombo vya habari na wasanii kwa nafasi zao kuendelea kutoa hamasa na elimu juu ya tukio hilo muhimu.

Uzinduzi rasmi wa mpango wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 umefanyka jana septemba 14, 2021 katika uwanja wa Jamuhuri Jijini Dodoma ukiwa na kaulimbiu isemayo “sensa kwa maendeleo ,jiandae kuhesabiwa”.