Dodoma FM

Serikali yaanzisha ukaguzi wa mabasi ya abiria ili kubaini usafirishaji wa watoto wanao ishi na kufanya kazi mitaani

15 September 2021, 2:30 pm

Na; Mariam Matundu.

Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa kutokomeza watoto wanaoishi mitaani wameazimia kuanza ukaguzi wa magari ya abiria ili kubaini usafirishaji wa watoto kwa lengo la kuzuia ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Hayo yamefikiwa katika kikao cha pamoja cha Makatibu Tawala wa Mikoa, Makamanda wa Polisi na Wadau wanaoshughulika na kutokomeza watoto wanaoishi mitaani, kilichofanyika Jijini Dodoma.

Katika kikao hicho, wamekubaliana kuwa Jeshi la Polisi lianze kutambua watoto wote wanaoishi na kufanya kazi mitaani ili kuwarejesha kwenye familia zao na kuiomba Wakala wa usafirishaji LATRA na Wadau wa usafiri kuweka mfumo madhubuti wa usafirishaji watoto.

Wamesema ukaguzi wa vyombo vya usafiri hautahusisha ubovu tu wa magari bali pia kwenye Chesesi ili kubaini usafirishaji wa watoto na ikiwezekana kuwekwa utaratibu wa kuandika umri wa wasafiri.

Aidha, Wadau hao wamesisitiza Jamii kuhamasishwa zaidi kuhusu malezi, matunzo na ulinzi wa watoto kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo vyombo vya Habari na nyumba za Ibada.

Kwa upande wake Kamishna wa Utawala na Rasilimali watu Kamanda Benedict Wakulyamba ameishukuru Wizara kwa kuwashirikisha wakiwa ni Wadau muhimu katika kumaliza changamoto hiyo kwani Jeshi la Polisi linahusika moja kwa moja na makundi yanayoshughulikiwa na Wizara na jukumu lao ni kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha kutokomeza tatizo hili.

Akihitimisha kikao hicho Katibu Mkuu Dkt. Jingu, amesema kuna kila sababu ya kuwalea watoto vizuri ili kuondokana na changamoto hiyo na kuwahamasisha Wadau wote kuweka nia thabiti ya kupambana na tatizo hilo kikamilifu.

Akiwasilisha mada kuhusu haki ya mtoto, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria kutoka Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Lucy Saleko amesema Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inawataka wazazi kuwajibika kuwalinda watoto wao dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa aina yoyote vinginevyo watachukuliwa hatua.