Dodoma FM

Jamii imetakiwa kuacha dhana potofu ya kufikiria mwanamke hawezi kuongoza baadhi ya wizara

14 September 2021, 2:10 pm

Na; Benard Filbert.

Kufuatia Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kumteua Dokta Stergomena Tax kuwa waziri wa ulinzi na jeshi la Kujenga Taifa jamii imetakiwa kuondoa dhana potofu iliyopo kwenye jamii kuwa mwanamke hawezi kuongoza wizara hiyo.

Hayo yameelezwa na mchambuzi wa masuala ya kisiasa jijini Dodoma bwana Jawadu Mohamed wakati akizungumza na taswira ya habari kuhusu baadhi ya watu kuwa na wasiwasi kuwa mwanamke hawezi kupewa wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa nchini.

Bwana Jawadu amesema toka nchi inapata uhuru miaka 60 iliyopita haijawahi kutokea mwananmke akapewa nafasi kuongoza wizara ya ulinzi hivyo huku uteuzi huo ikizua mijadala miongoni mwa watanzania.

Kadhalika ameongeza kuwa wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga Taifa ni wizara yenye nidhamu hivyo hakutokuwa na changamoto kubwa kama wizara zingine.

Jana Rais Samia aliwaapisha baadhi ya mawaziri ambao alifanya marekebisho katika baraza lake akiwepo waziri wa ulinzi Dokta Stergomena Tax na katika hotuba yake alinukuliwa akisema ameamua kuvunja miiko na dhana iliyojengeka katika jamii kuwa mwanamke hawezi kuongoza wizara hiyo kitu ambacho sio kweli.