Dodoma FM

Jamii yaaswa kuepuka matumizi ya sigara wakati huu wa mapambano dhidi ya uviko 19

13 September 2021, 11:55 am

Na; Shani Nicolous.

Wito umetolewa kwa jamii kuepuka uvutaji wa sigara hususani wakati wa mapambano dhidi ya UVIKO 19.

Akizungumza na Taswira ya habari Dr. Missani Yango kutoka hospitali ya mkoa amesema kuwa sigara ina mchango mkubwa katika kueneza ugonjwa wa Corona kwani inaweza kuchochea pia magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza.

Amesema kuwa wavutaji wa sigara mara nyingi hutumia mfumo wakugusagusa viungo vya mwili kama mdomo kwa kuwasha sigara hivyo kusababisha usambaaji wa virus vya Corona .
Ameongeza kuwa sigara inasababisha kupunguza kinga za mwili hivyo ni rahisi kupata ugonjwa hatarishi wa mapafu ulio mkali zaidi.

Aidha amesema kuwa mtu yoyote anaetaka kuacha kuvuta sigara anaweza kupunguza idadi ya sigara kwa siku, kuchelewa kuvuta kuliko kawaida ya siku zote na njia nyingine.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi jijini Dodoma wamesema kuwa sigara si nzuri kiafaya ni vema wavutaji wakatafuta namna ya kukata kiu hiyo kiafya kuliko kuathiri afya zao .

Serikali kupitia wizara ya afya inaendelea kutoa elimu mbalimbali nchini juu ya namna bora ya kuishi kwa kuepuka maambukizi ya Uviko 19 hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kufuata maelekezo husika ili kulinda afya .