Dodoma FM

EWURA yatangaza kupanda kwa bei ya mafuta

1 September 2021, 12:44 pm

Na;Mindi Joseph .

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kupanda kwa bei za mafuta kutokana na kubadilika kwa bei katika Soko la Dunia na gharama za uagizaji.

Bei ya mafuta kupanda itaanza kutumika kuanzia leo Septemba Mosi kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo katika soko la Dunia.

Akizungumza na Taswira ya habari Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo, amesema katika bandari ya Dar es Salaam bei ya petroli imeongezeka kwa shilingi 84, dizeli shilingi 29 na mafuta ya taa bei imeongezeka kwa shilingi 18.

Katika bandari ya Tanga bei ya petroli imeongezeka kwa shilingi 53, dizeli shilingi 14 na ya mafuta ya taa itabaki kama ilivyokuwa na EWURA imesema katika bandari ya Mtwara petroli imeongezeka shilingi 108 na dizeli shilingi 46.

Aidha katika Mikoa mingine Bei ya mafuta itategemea na wahusika wanachukulia wapi mafuta hayo kati ya bandari hizo, lakini bei ni elekezi.

Dodoma fm imezungumza na baadhi ya madereva wa daladala katika jiji la Dodoma wanaofanya shughuli zao katika stendi ya Sabasaba na wamelalamikia upandishwaji wa bei hizo za mafuta kwani hazijazingatia maslahi yao