Dodoma FM

Ugonjwa wa uviko 19 watajwa kuathiri nguvu za kiume

31 August 2021, 11:35 am

Na; Selemani Kodima.

Imeelezwa kuwa athari mojawapo anayoipata Mtu aliyepata Virusi vya Ugonjwa wa Uviko-19 ni pamoja na upungufu wa nguvu za kiume.

Hili linajiri baada ya Hivi karibuni ripoti ya utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Miami nchini Marekani kueleza kuwa zipo athari zinazotokana na Virusi hivyo hali ambayo vinaathiri zaidi mishipa ya damu hasa ile inayopeleka damu moja kwa moja kwenye uume.

Kutokana na hilo ,Taswira ya habari imezungumza na Dkt Baraka Nzobo kutoka Wizara ya Afya Idara ya Kinga, kitengo cha ithemolojia na udhibiti wa magonjwa amesema kwa mujibu wa utafiti huu ni kweli zipo athari ambazo zinasababishwa na kuganda kwa Damu kwenye Mishapa ya Damu ikiwa ni pamoja na mishipa ya Uume.

Dkt Nzobo amesema kiungo kingine kinachoathiriwa ni pamoja Moyo ambao kazi yake kubwa ni kusuma damu katika maeneo yote ya mwili hivyo uwezekano wa msukumo wa damu kushindwa kufanya kazi katika mishipa ya Uume.

Aidha amesema jambo hilo sio la nadharia bali ni hali halisi ya kirusi hicho ambapo amesema baadhi ya wanaume wamekuwa wakiripoti visa vya upungufu wa nguvu za kiume katika hospitali mbalimbali .

Hata hivyo Dkt Nzobo amesema ipo haja jamii kujikinga na kuchukua tahadhari pamoja na kupokea chanjo ili kujiepusha na athari zinazotokana na kirusi cha Corona.

Kwa mujibu wa jarida la World Journal of Men’s Health la Marekani, tafiti zaidi zimebaini kuwa kuharibiwa kwa mishipa ya damu kwenye uume wa wagonjwa wa Uviko-19 imethibitishwa baada ya kufanya uwiano na wengine wawili ambao hawajaathiriwa na Uviko-19 ambao tayari walishapata tatizo hilo.