Dodoma FM

Jamii yaaswa kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi

17 August 2021, 11:33 am

Na; Alfred Bulahya.

Imeelezwa kuwa watoto wasiopungua 10 wameuawa kutokana na kupigwa na kuchomwa moto ndani ya jiji la Dodoma katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kitendo ambacho kinatajwa kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Hayo yamebainishwa leo na Bw Ibrahim Mtangoo ambaye ni msimamizi na mfanyakazi kitengo cha watoto wanaoishi mtaani kutoka shirika la KISEDETI linalojishughulisha na masuala ya huduma za watoto na vijana wanaoishi na kufanyakazi mtaani.

Aidha amesema kwa sasa hali inaendelea kuimarika kutokana na elimu inayotolewa na wadau mbali mbali ikiwemo KISEDETI hivyo ni wakati sasa wa mamlaka kuchukua hatua kali kwa wanaobainika kukiuka haki za binadamu huku akiiasa jamii kuheshimu haki za binadamu.

Mratibu kutoka shirika hilo Mandago Mkama amesema kuna haja ya jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake ijenge tabia ya kufuata sheria kama zinavyoelekeza ili kuepusha kuendelea kwa vitendo vya uvunjifu wa amani ambao hutokana na watu kulipiza visasi baada ya kufanyia ukatili.

Aidha amesema iwapo jamii itaendelea kujichukulia sheria mkononi kuna uwezekano mkubwa wa kuja kuwa na taifa lenye watu wasiotii sheria bila shuruti hali ambayo itachangia ongezeko la vitendo vya uvunjifu wa amani.