Dodoma FM

Serikali yaja na mpango wa kupunguza tozo za leseni kwa radio za jamii katika ngazi za wilaya na mipakani

26 July 2021, 11:31 am

Na; Mariam Matundu.

Katika kuboresha huduma za mawasiliano kwa umma hususani kwa njia ya Redio wizara ya teknolojia ya habari na mawasiliano imesema inampango wa kupunguza tozo za leseni kwa radio za kijamii katika ngazi ya wilaya na maeneo ya mipakani.

Hayo yamesemwa na Waziri wa wizara hiyo Dkt Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa Redio jamii iliyoanzishwa na shirika la utangazaji la taifa TBC kwa kushirikiana na mfuko wa mawasiliano kwa wote UCSAF hii leo jijini Dodoma ambapo amesema kuwa kwa kufanya hivyo kutawezesha wananchi katika ngazi ya jamii wapate haki ya kupata habari.

Nae naibu waziri wa wizara ya habari,utamaduni, ,sanaa na michezo Pauline Gekul amewataka waandishi wa habari kuzingatia weledi na maadili wakati wakifanya shuguli zao na kusisistiza kuendelea kuwatumia wataalamu ili kuelimisha jamii juu ya janga la CORONA.

Awali mtendaji mkuu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote UCSAF Justina Mashiba amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha ufikishwaji wa taarifa za utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya serikali kwa wananchi kwa urahisi na usahihi kwa njia ya kisasa.

Mfuko wa mawasiliano kwa wote UCSAF umeingia makubaliano ya TBC ya ukarabati wa studio za kisasa za radio jamii ambapo mfuko umetoa zaidi ya bilioni moja ili kufanikisha ukarabati huo huku kukiwa na makubaliano ya kuboresha usikivu katika wilaya zaidi ya kumi hapa nchini ambapo ufuko umetoa zaidi ya bilioni tatu.