Dodoma FM

Mkuu wa mkoa wa Dodoma ameitaka Benki ya mwalimu(MCB) kuwasaidia walimu kupata mikopo yenye masharti nafuu

23 July 2021, 12:11 pm

Na; Mindi Joseph.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ameitaka benki ya Mwalimu kuwasaidia walimu nchini kupata mikopo yenye masharti nafuu.

Akizungumza jijini Dodoma wakati akizindua mpango wa mikopo ya mashine za uzalishaji mali ujulikano kama Mwalimu na Ujasiriamali amesema kuwa walimu wengi nchini wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na aina ya mikopo wanayokopa kutoka katika taasisi ambazo zina masharti magumu na riba kubwa.

Aidha amesisitiza kuwa ifike hatua benki ya Mwalimu itazame vipi inakuja na utofauti gani na taasisi nyingine za kifedha ili muweze kuwakopesha walimu wenye uhitaji wa fedha kwa ajili ya kufanya mambo mbalimbali yanayo wakabili bila kuwapatia usumbufu wowote.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Mwalimu (MCB) ,Richard Makungwa amesema katika jitihada za kuunga mkono Serikali kwenye kukuza sekta ya viwanda na biashara Benki itawawawezesha walimu,watumishi wa Serikali pamoja na umma kuweza kukuza na kuwajengea uwezo kupitia shughuli za ujasiriamali ili kuwakwamua kiuchumi.

Naye Naibu katibu Mkuu wa chama cha walimu (CWT) Japhet Maganga amesema kuwa wao kama walimu na watumishi wengine wapo tayari kutoa uahirikiano katika kuhakikisha kwamba benki hiyo inaleta manufaa chanya kwa walimu na hata jamii nzima kwa ukubwa wake.