Dodoma FM

Wakazi Wilayani Chamwino watakiwa kutunza na kusimamia miradi ya maji

16 July 2021, 12:48 pm

Na; Benard Filbert.

Wakazi katika wilaya ya Chamwino wametakiwa kutunza na kuisimamia miradi ya maji ambayo imekuwa ikiratibiwa na wakala wa huduma za maji vijijini RUWASA ili kuepusha changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Hayo yameelezwa na meneja wa RUWASA Wilaya ya Chamwino Bi. Christina Msengi wakati akizungumza na taswira ya habari kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji katika Wilaya hiyo.

Amesema ndani ya Wilaya hiyo kuna miradi ambayo inatekelezwa katika kata mbalimbali ikiwemo kata ya Dabalo kijiji cha Chiwondo ambapo wana miradi 3 kwa ambayo inatekelezwa kwa kushirikiana na Innovation Africa.

Ameongeza kuwa miradi mingi ya maji katika Wilaya hiyo inakabiliwa na ukosefu wa nishati ya umeme wa TANESCO jambo ambalo linawalazimu kutumia nishati ya umeme wa jua ambao wakati mwingine umekuwa kikwazo katika kutekeleza majukumu yao.

Aidha Bi. Christina amewataka wananchi kuondoa wasiwasi wa kutumia maji ya chumvi kwani yamefanyiwa vipimo na shirika la afya Duniani WHO na kuthibitishwa kuwa hayana athari kiafya.

Ikumbukwe kuwa maji ni uhai hivyo upatikanaji wa maji unachagiza uwepo wa maendeleo ndani ya jamiii.