Dodoma FM

Wakazi wa Chiwondo walazimika kutembea kilomita 6 kutafuta maji

15 July 2021, 11:53 am

Na; Benard Filbert.

Changamoto ya ukosefu wa maji katika kijiji Cha Chiwondo Kata Ya Dabalo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma imetajwa kuwa kikwazo cha maendeleo kwa wakazi hao kutokana na kutembea zaidi ya kilomita 6 kutafuta huduma hiyo.

Wananchi hao wameiambia Dodoma fm kuwa kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama kunawalazimu wakazi hao kutumia maji ya mabwawa ambayo yanaathari kiafya.
Wamesema uongozi wa kata yao hauna dalili zozote za kutatua changamoto hiyo huku changamoto hiyo ikiwakabili tangu kuanzishwa kwa kijiji.

Filipo Ainea afisa mtendaji wa kijiji cha Chiwondo amesema licha ya uwepo wa changamoto hiyo kuna wafadhili wa Innovation Africa ambao wamechimba visima 3 katika vitongoji 3 hatua iliyosaidia kupunguza makali ya changamoto hiyo.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Dabalo Bw. Isihaka Rajab amekiri uwepo wa changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama ndani ya kata hiyo ingawa tayari wameongea na wafadhili tofauti ambao watachimba visima na kumaliza tatizo hilo.

Serikali inaendelea na juhudi za kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa kila kijiji hivyo wananchi wanaombwa kuwa wavumilivu ili kuipa Serikali muda wa kutosha kushughulikia changamoto hiyo katika maeneo mbalimbali.