Dodoma FM

Ugumu wa maisha na msongo wa mawazo ni sababu zinazopekea vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya

14 July 2021, 12:49 pm

Na;Yussuph Hans.

Ugumu wa maisha na msongo wa mawazo bado vimeendelea kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea wimbi la baadhi ya vijana kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya.

Wakizungumza na taswira ya habari baadhi ya vijana waliokuwa watumiaji wa dawa za kulevya wamesema inawawia vigumu vijana wengi kuacha matumizi ya dawa hizo kutokana na sababu mbalimbali huku wengine wakiamini kuwa wanaweza kumaliza changamoto za maisha zinazowakabili.

Kituo hiki kimezungumza na daktari kutoka hospitali ya afya ya akili Mirembe kitengo cha tiba ya waathirika wa dawa za kulevya Dokta. Rehema Chaki na amesema mara nyingi vijana hutumia dawa za kulevya katika kipindi cha kubalehe na wengi huwa na magonjwa ya akili yanayotokana na msongo wa mawazo.

Kwa upande wake Mgeni Mussa ambae ni muuguzi kutoka kitengo cha tiba mbadala dawa za kulevya amesema kuwa ni wajibu wa wazazi kuhakikisha wanakuwa karibu na watoto wao katika kipindi chote na kuwa na utamaduni wa kuwachunguza mtindo wao wa maisha.

Matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa yakishamiri kwa vijana wa rika mbalimbali kutokana na makundi rika, msongo wa mawazo katika familia nakadhalika.