Dodoma FM

Serikali yatatua changamoto ya umeme kata ya Membe

8 July 2021, 11:32 am

Na; Benard Filbert.

Miezi kadhaa baada ya Dodoma FM kuripoti habari kuhusu changamoto ya kukosekana kwa nishati ya umeme katika kata ya Membe Wilayani Chamwino hatimaye Serikali imeanza kuchomeka nguzo za umeme.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Chitaburi wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo kwani toka kuanzishwa kwa Kata hiyo hawajiwahi kutumia nishati ya umeme.

Mmoja wa wakazi hao Juma Kangae ameipongeza Dodoma fm kwa kurusha changamoto mbalimbali zinazowakabili katika Kata hiyo likiwepo suala la ukosefu wa umeme jambo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu katika kata hiyo.

Amesema endapo huduma hiyo itafanikiwa kama inavyotakiwa itasaidia katika mambo mbalimbali yamaendeleo ikiwemo vijana kujiajiri.

Taswira ya habari imezungumza na Diwani wa Kata ya Membe Bw. Simon Mcheo na amesema hatua za mwanzo zimeanza ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hiyo lakini kipaumbele kikubwa ni kwenye taasisi zilizopo katika Kata hiyo.

Hivi karibuni Waziri wa nishati Medard Kalemani alinukuliwa akisema huduma ya umeme itamfikia kila mwananchi pasipo kujali ni maeneo ya mijini au vijijini.