Dodoma FM

Rais Samia azitaka taasisi za Dini nchini kufanya kazi kwa kuaminiana

8 July 2021, 11:49 am

Dawati la Habari.

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za dini Nchini kufanya kazi kwa uwazi na kuaminiana ikiwemo kuweka wazi mahesabu ili watoza kodi waweze kujua hali halisi ya uendeshaji wa taasisi hizo.

Rais Samia ameyasema hayo leo katika mkutano mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania – CCT uliofanyika Mkoani Morogoro na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa jumuiya hiyo Nchini wakiwemo viongozi wa Mkoa wa Morogoro

Amesema kufanya kazi kwa uwazi ni pamoja na kuruhusu ukaguzi wa mahesabu ili watoza kodi waweze kukagua na kujua uhalisia wa uendeshaji wa huduma hizo katika jamii ikiwemo elimu pamoja na afya kupitia fedha ambazo wakati mwingine zimekuwa zikitolewa na wafadhili.

Rais Samia amesema wakati mwingine Serikali imekuwa ikilazimika kutoza kodi kwa taasisi hizo kutokana na kujitokeza kwa ushindani wa huduma swala ambalo linadhihirisha wazi kuwa baadhi ya taasisi hizo zipo kibiashara zaidi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa jumuiya Kikristo Tanzania (CCT) Askofu Dr. Aliniksya Cheyo amempongeza Rais Samia kwa utumishi wake ndani ya siku 100 ambazo amefanikiwa kutekeleza mambo mbalimbali ikiwemo kudumisha amani ya Nchi, umoja wa kitaifa pamoja na kufungua milango ya kuimarisha zaidi uchumi wa Nchi.

Rais Sami Suluhu Hassan anaendelea na ziara yake ya siku mbili Mkoani Morogoro