Dodoma FM

Kampeni ya zero migogoro yafanikiwa kusikiliza kesi zaidi ya elfu moja kwa siku mbili

8 July 2021, 11:11 am

Na; Shani Nicolous.

Kampeni ya zero migogoro ya ardhi Mkoani Dodoma imefanikiw kusikiliza kesi zaidi ya elfu moja kwa siku mbili huku baadhi ya kesi zikitatuliwa papo kwa papo na nyingine zilizohitaji kufika maeneo husika zikiendelea kufanyiwa kazi.

Akizungumza na Dodoma fm mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Jabil Shekimweli amesema kampeni hiyo itasaidia kumaliza baadhi ya changamoto zilizoleta shida kwa muda mrefu kutokana na utaratibu mzuri na Mifumo rafiki inayotumika kutatua changamoto hizo.

Amesema ni fursa ya kila mwananchi wa Mkoa wa Dodoma mwenye tatizo hilo kufika maeneo husika kwani bado milango ipo wazi kwa ajili ya kuendelea kusikiliza na kutatua changamoto za migogoro ya ardhi.

Ameongeza kuwa kampeni hiyo ni kwa ajili ya Mkoa mzima wa Dodoma hivyo wameanza na Wilaya ya Dodoma mjini na baada ya hapo utaratibu mwingine utatangazwa kwa ajili ya kutembelea Wilaya zote hivyo wananchi watumie muda huu vizuri kutatua changamoto zao.

Nao baadhi ya wananchi jijini hapa wamesema kuwa wamechoshwa na kero za migogoro ya ardhi zilizotafutiwa ufumbuzi kwa muda mrefu hivyo kupitia kampeni hii imani yao nikumaliika kwa migogoro hiyo.

Aidha wameiomba serikali kutembelea maeneo yenye migogoro kuliko kumalizia maofisini kwani hiki ndiyo chanzo cha migogoro hiyo kutokumalizika.

Kampeni hiyo itaendelea kuanzia kesho mpaka itakapofikia mwisho July 14 mwaka huu ambapo kwa kesho timu nzima itakuwa Mtumba,Chikombo,Ihumwa na Nzuguni, na tarehe tisa timu hiyo itakuwa Chahwa,Ipala, Hombolo bwawani na Hombolo Makulu na siku zinazofuata kata nyingine zitaendelea.