Dodoma FM

Watumishi wa wizara za maji na mamlaka zake watakiwa kuwa na lugha nzuri kwa wateja

6 July 2021, 12:15 pm

Na; Pius Jayunga.

Waziri wa maji Jumaa Aweso amewataka watumishi wa Wizara ya maji na mamlaka zake kuwa na lugha nzuri kwa wateja wao ili kuchochea utoaji wa huduma bora za maji kwa wananchi maeneo mbalimbali Nchini.

Kauli hiyo ameitoa leo Jijini Dare s salaam wakati akifunga kikao cha DAWASA cha mwaka 2020/21 na kuanza 2021/22 katika mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi kwa kuwa na kauli nzuri wanapohudumia wateja wa maji.

Amezitaka mamlaka kuainisha gharama halisi za uunganishiji wa huduma za maji ikiwa ni pamoja na kuepuka ubambikiziaji wa bili za maji kwa wananchi na kwamba ni haki ya mteja wa maji kushirikishwa katika usomaji wa mita za maji ili aelewe kiwango chake cha matumizi na kiasi cha pesa anachotakiwa kulipia.

Kwa mjibu wa Waziri Aweso katika bajeti ya mwaka 2021/22 Bunge limeiidhinishia Wizara hiyo fedha kiasi cha shilingi Bilioni 680 zitakazotumika kutatua changamoto ya maji wakati huo Rais Mh. Samia suluhu Hassan akiwa ameiongezea fedha wizara ya maji kiasi cha Bilioni 207.

Kutokana na kuidhinishiwa fedha hizo Wizara ya maji inatarajia kwenda kutekeleza miradi 1527 maeneo ya Vijijini na miradi 114 maeneo ya mjini.