Dodoma FM

Wakazi Mkutani walazimika kutembea kilomita sita kutafuta maji

6 July 2021, 11:49 am

Na; Benard Filbert.

Wakazi wa Kijiji cha Mkutani Kata ya Hogoro Wilayani Kongwa wanakabiliwa na changamoto ya huduma ya maji safi na salama hali ambayo imekuwa ikiwalazimu kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.

Hayo yameelezwa na wakazi hao wakati wakizungumza na taswira ya habari ambapo wamebainisha kuwa changamoto hiyo imekuwa kubwa kwani inawalazimu kutembea umbali zaidi ya kilomita 6 kufuata huduma ya maji.

Wamesema kutokana na usumbufu wakutembea umbali mrefu umekuwa ukiathiri maisha yao kwani baadhi yao wamekuwa wakishindwa kutembea umbali huo kufuata huduma hiyo.

Ezekiel Masima Mwenyekiti wa kitongoji Cha Mkungugu Kijiji cha Mkutani amesema changamoto ya maji ni ya muda mrefu licha ya kuhimiza viongozi kutatua changamoto hiyo.

Hata hivyo Diwani wa kata ya Hogoro Bw. Mtwangaa Samira amesema hivi karibuni anatarajia kufanya ziara ya kuzungukia vijiji vyote katika Kata hiyo ili kujua ukubwa wa changamoto hiyo na kuanza mikakati ya skutatua suala hilo.

Upatikanaji wa huduma ya maji Nchini bado ni kilio kwa wakazi wengi hususani maeneo ya Vijijini.