Dodoma FM

Baadhi ya wafanyakazi wa ndani waelezea kukumbana na changamoto ya ukatili na unyanyasaji kutoka kwa waajiri wao

6 July 2021, 2:01 pm

Na;Yussuph Hans.

Imeelezwa kuwa licha ya mchango mkubwa katika Familia, bado wafanyakazi wa ndani wanakabiliwa na changamoto ya kufanyiwa vitendo vya Ukatili na Unyanysaji wa kijinsia kutoka kwa waajiri wao, wanafamilia, ndugu na marafiki.

Mmoja wa wasaidizi wa kazi za ndani Jijini Dodoma ambae hakutaka jina lake litajwe amesema baadhi ya waajiri wamekuwa wakikiuka makubaliano ya kufanya kazi za ndani na hivyo kupewa majukumu mazito yaliyo juu ya uwezo wao.

Ameongeza kuwa pamoja na waajiri kuwafanyisha kazi nzito pia wamekuwa wakifanyishwa biashara ya Ngono na wakati mwingine Vijana wao wa Kiume kuwataka kimahusiano.

Jelda Luyangi Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya Dodoma amesema kuwa matukio hayo yamekuwa yakishughulikiwa kwa kufuata Sheria na Kanuni ambapo ni wajibu wa watu wa karibu pamoja na muhusika mwenyewe kutoa Taarifa za vitendo hivyo.

Aidha amewaomba waajiri kuacha kuwafanyia vitendo vya Ukatili Wafanyakazi wa Ndani kwa kuwapa adhabu kali ikiwemo kutowalipa mshahara, hali inayopelekea kufanya ukatili kwa Watoto wao na hivyo wawachukulie kama sehemu ya Familia.

Nao baadhi ya waajiri wa Wasaidizi wa ndani wamekiri kuwepo kwa Matukio hayo huku wakitoa wito kwa Jamii kuhakikisha wanawahafamu vyema Wasaidizi wa ndani wanaowaajiri.

Kumekuwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na mashirikia ya kutetea haki za watoto na wasichana Nchini, lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo wa kutambua Wajibu, Haki na Sheria zinazowalinda Watoto hao ili waweze kijisimamia wenyewe dhidi ya Unyonywaji na unyanyaswaji wanaoweza kukumbana nao.