Dodoma FM

Wakazi wa Mlebe walia na changamoto ya upungufu wa madawa na wahudumu wa Afya

5 July 2021, 9:49 am

Na; Victor Chigwada.

Wananchi wa kijiji cha Mlebe Kata ya Msamalo wanakabiliwa na uhaba wa wahudumu wa afya katika zahanati yao hali inayodhoofisha utoaji wa huduma za matibabu hasa kwa akina mama wajawazito.

Baadhi ya wananchi hao wakizungumza na taswira ya habari wamesema kuwa kuwepo kwa Daktari mmoja na nesi mmoja katika zahanati hiyo kunapelekea wagonjwa kuto pata huduma kikamilifu hususani akina mama wajawazito huku upatikanaji wa dawa katika zahanati hiyo ukiwa hautoshelezi.

Mwenyekiti wa kijiji hichi Bw.Joseph Mpilimi amekiri kuwepo kwa uhaba wa wahudumu wa afya katika zahanati hiyo huku upatikanaji dawa ukiwa ni changamoto kwani wanapo agiza dawa huletewa dawa tofauti na bajeti waliyo agiza.

Naye Diwani wa Kata hiyo Bw.Eliasi Kaweya amesema kuwa tayari walisha fanya maombi kwa DMO kwaajili ya kuongezewa mtumishi mmoja na tayari vituo vimeshapewa fedha ya kununulia madawa.

Zahanati nyingi nchini hususani za vijijini zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya uhaba wa madawa pamoja na wahudumu wa afya ikiwemo madaktali pamoja na manesi.