Dodoma FM

Wakazi wa kata ya Iduo waiomba serikali kufanya marekebisho ya barabara

5 July 2021, 12:31 pm

Na; Beanard Filbert.

Wakazi wa kata ya Iduo Wilayani Kongwa wameiomba Serikali kuhakikisha wanafanya marekebisho ya miundombinu ya barabara katika Kata hiyo ili kuepusha usumbufu ambao wamekuwa wakikutana nao hususani katika msimu wa mvua.

Hayo yameelezwa na wakazi hao wakati wakizungumza na taswira ya habari ambapo wamebainisha kuwa barabara hizo zimekuwa zikiwasaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo hivyo ni vyema viongozi wao wakafanya marekebisho katika kipindi hiki.

Wameongeza kuwa endapo miundombinu hiyo itarekebishwa itasaidia shughuli za maendeleo kufanyika kwa kipindi chote cha mwaka.

Taswira ya habari imezungumza na Diwani wa Kata ya Iduo Bw. Valentino Senyinda na amekiri uwepo wa changamoto hiyo katika kata yake ikiwemo barabara ya Masinyeti kwenda Ihanda.

Amesema utekelezaji wa marekebisho ya barabara hizo utaanza hivi karibuni baada ya kukaa kikao cha mwisho na wakala wa barabara mijini na vijiji TARURA.

Kadhalika amewaomba wakazi wa kata hiyo kuwa wavumilivu kwani lengo lao ni kutatua changamoto hiyo ambayo imekuwepo kwa muda mrefu.