Dodoma FM

Wizara ya Elimu Tanzania kupitia taasisi ya (TET) yaandaa mkutano wa kupokea maoni kutoka kwa wadau

25 June 2021, 1:13 pm

Na; Rabiamen Shoo.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imeandaa mkutano wa kupokea maoni kutoka kwa wadau wa elimu kuhusu uboreshwaji wa Mitaala ya Ngazi ya Elimu ya Awali,Msingi na Sekondari. 

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma hapo kesho Juni 26, 2021na utazinduliwa na Waziri wa elimu,Sayansi na teknolojia Prof. Joyce Lazaro Ndalichako.

Akizungumza mapema leo katika kipindi cha Dodoma Live kinachorushwa hapa Dodoma Fm, Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt.Aneth Komba amesema mkutano huo umeitishwa kutokana na wadau kudai mtaala uliopo sasa hautoi ujuzi.

Dkt.Komba amesema njia mbalimbali zitatumika katika kutoa maoni hayo ambapo watatoa nafasi kwa kila mtu kushiriki ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii.

Naye Dkt.Godson Lema kutoka taasisi ya Elimu Tanzania amesema mkutano huu unalenga wadau kutoka sekta mbalimbali na hakutakuwa na kiingilio chochote.

Taasisi ya Elimu Tanzania TET ipo chini ya Wizara ya elimu,Sayansi na teknolojia ambapo inajishughulisha na kuandaa mitaala,kuandaa vifaa saidizi vya mitaala,kufanya utafiti na kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu ubora wa elimu na kutoa mafunzo endelevu kwa walimu kazini.