Dodoma FM

Rais Samia Suluhu amewataka viongozi wa dini Nchini kuendeleza mapambano dhidi ya janga la corona

25 June 2021, 1:49 pm

Na; FRED CHETI.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassani leo June 25 amewataka viongozi wa dini nchini kuendeleza mapambano dhidi ya janga la Corona.

Akizungumza wakati akihutubia baraza la Maaskofu wa jimbo katoliki Tanzania jijini Dar es salaam Mh. Rais amewataka viongozi hao kuendelea kuliombea Taifa pamoja na kuwahimiza waumini wao kuendelea kuchukua tahadahari juu ya ugonjwa wa Covid 19 ili kuepuka maambukizi mapya kwa kuwa bado ugonjwa huo upo.

Aidha Mh. Rais amezipongeza taasisi za dini nchini ikiwemo kanisa Katoliki Tanzania zinazotoa huduma mbalimbali kwa watanzania zikiwemo afya na elimu ambapo amesema Serikali inatambua umuhimu wa taasisi hizo katika kulijenga Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya maaskofu, askofu wa kanisa Katoliki nchini anayehudumia kama askofu msaidizi wa Jimbo la Bukoba Method Kilaini ameiomba serikali kurejea nia yake ya awali iliyozisukuma taasisi za dini kuwekeza katika sekta ya elimu na afya kwa kufanya marekekebisho ya sera inazozibana ili ziendelee kutoa huduma nzuri kwa watanzania.

Huu ni Muuendelezo wa Rais Mh.Samia Suluhu Hassan kuendelea kukutana na makundi mbalimbali ambapo leo june 25 amekutana na kuzungumza na Baraza na Maaskofu wa Jimbo Katoliki Tanzania jijini Dar es Salaam.