Dodoma FM

Iyumbu waishukuru serikali kwa kusimamia ipasavyo migogoro ya Ardhi

25 June 2021, 2:07 pm

Na; Victor Chigwada.

Wananchi wa Kata ya Iyumbu jijini Dodoma wameishukuru Serikali kwa kusimamia ipasavyo utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Baadhi ya wanachi hao wakizungumza na taswira ya habari wamesema tangu Diwani wa Kaya yao alipoingia madarakani ameshirikiana na wananchi pamoja na viongozi wengine kutafutia ufumbuzi changamoto hiyo iliyokuwa ya muda mrefu.

Mwenyekiti wa mtaa wa Nyerere Bw.Ayubu Mandabaga amekiri kuwa awali Iyumbu ilikuwa ikikabilia na migogoro ya ardhi ya mara kwa mara lakini mpaka sasa asilimia kubwa wameitatua chini ya usimamizi wa diwani wao.

Naye Diwani wa Kata hiyo Bw. Eliasi Situchi amesema alikuta migogoro kadhaa ya ardhi katika Kata hiyo ambayo ilikuwa imedumu kwa muda mrefu lakini wamejitahidi kuleta utengamano kwa kukaa na wananchi kutafuta ufumbuzi.

Ameongeza kuwa kwa sasa wapo katika hatua ya ugawaji viwanja kupitia mradi wa upimaji shirikishi pamoja na kuwepo kwa changamoto ndogo zinazohitaji marekebisho.

Migogoro ya ardhi imekuwa ikiibuka katika maeneo mbalimbali nchini Serikali kupitia viongozi wa maeneo husika imeendelea kuzitatua kadri inavyowezekana.