Dodoma FM

Tanzania yafikia 90% ya udhibi wa dawa za kulevya

23 June 2021, 11:25 am

Na; Mindi Joseph

Kuelekea siku ya kimataifa ya kupambana na dawa za kulevya Tanzania imetajwa kufikia zaidi ya asilimia 90 ya udhibiti na kupambana na dawa hizo.

Hii ni kwa mujibu wa Riporti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (​UNODC) ya mwaka 2019/20.

Akizungumza leo Jijini Dodoma Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya Nchini Gerald Musabila Kusaya amesema hali hii inaonesha udhibiti wa dawa za kulevya nchini umekuwa mkubwa kwani kilo 859.36 zimekamatwa kwa mwezi Aprili ikiwa ni kiasi kikubwa kuwahi kukamatwa nchini.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka amesema Mkoa unaendelea kudhibiti dawa za kulevya licha ya Wilaya ya Mpwapwa kutajwa kujihusisha zaidi na kilimo cha dawa hizo huku Kondoa ikitajwa kuwa ni njia ya kupitisha mihadarati.

Aidha Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kujitokeza katika wiki ya kupambana na dawa za kulevya ambayo kitaifa inafanyika jijini Dodoma katika viwanja vya mwalimu Nyerere na amevitaka vyombo vya habari kushiriki pamoja katika kutokomeza dawa za kulevya.

Juni 26 kila mwaka ni siku ya kimataifa ya kupambana na utumiaji na biashara haramu ya dawa za kulevya na Umoja wa Mataifa umeitenga siku hii kuuhimiza ulimwengu kupambana na janga hili ambalo linaathiri binadamu na Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Tuelimishane juu ya tatizo la dawa za kulevya kuokoa Maisha.