Dodoma FM

Serikali inakamilisha mkakati wa huduma ya mazoezi tiba nchini

23 June 2021, 11:52 am

Na; Yussuph Hans

Serikali imesema inakamilisha mpango mkakati wa kutoa huduma ya mazoezi tiba nchini, kufuatia kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo ikiwemo walio na ugonjwa wa kupooza.

Hayo yamebainishwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh.Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mh.Dkt Alice Kapungi Kaijange aliyehoji nini mpango wa Serikali katika kutatua ongezeko la Wagonjwa wanaohitaji huduma ya mazoezi tiba katika Vituo vya Afya.

Mh.Dugange amesema kuwa Wizara ya Afya imefanya tathimini ya mahitaji ya huduma ya Mazoezi Tiba na utengamao katika Vituo vya Afya na kukamilisha mpango utakaotoa mwongozo wa kutatua changamoto hiyo.

Ameongeza kuwa kuna hatua mbalimbali wanazoendelea kufanya kwa sasa huku wakiangalia namna ya kuboresha huduma hiyo ili iweze kupatikana katika Mfumo wa Bima za afya kubwa (NHIF) na Bima ndogo (CHF).

Katika hatua nyingine Mh.Dugange amesema kuwa Serikali inapitia na kuboresha sera ya ujenzi wa Zahanati kila Kijiji na Kituo cha Afya kwa kila kata ili Ujenzi ufanyike kimkakati.

Bunge limeendelea leo Jijini Dodoma baada ya kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo leo ni kikao cha hamsini na saba, mkutano wa tatu wa Bunge la 12.