Dodoma FM

Wakazi wa kata ya kikombo waiomba serikali kumalizia mradi wa umeme ulionza tangu 2018

22 June 2021, 1:46 pm

Na; Victor Chigwada.

Wananchi wa Kata ya Kikombo jijini Dodoma wameiomba Serikali kuwakamilishia mradi wa umeme ambao ulianza tangu mwaka 2018 kwa kuwa baadhi ya maeneo bado hayajafikiwa na huduma hiyo.

Baadhi ya wananchi hao wakiwemo wa Mtaa wa Chololo wameiambia taswira ya habari kuwa ni muda mrefu tangu waliposimamishiwa nguzoza umeme hali iliyoamsha matumaini lakini hadi leo bado hawajaunganishiwa huduma hiyo.

Mwenyekiti wa mtaa huo Bw. Maiko Mbumi amekiri kuwepo kwa kutofikiwa na mradi wa umeme wa REA, na kuwa kuna maeneo ambayo yalipelekewa nguzo muda mrefu ila bado hawaja unganishiwa mpaka sasa.

Naye Diwani wa Kata ya Kikombo Bw.Emmanuel Manyono amesema kuwa kwa asilimia kubwa tayari Kata yake ina umeme ila wanategemea kuelekeza nguvu yao katika mtaa wa Rusinde uliopo Chololo ambao bado haujafikiwa.

Pamoja na changamoto za umeme katika maeneo mbalimbali nchini Serikali kupitia wakala wa umeme vijijini REA imeendelea na juhudi za kuhakikisha kila Kijiji kinafikiwa na huduma hiyo.