Dodoma FM

Serikali kuboresha vitambulisho vya wajasiriamali ambavyo hutolewa kwa kipindi cha mwaka mzima

22 June 2021, 1:58 pm

Na;Yussuph Hans.

Serikali katika kuhakikisha wajasiriamali wadogo wanafanya biashara kwa uhuru, imesema inaendelea kuboresha vitambulisho vya wajasiriamali ambavyo hutolewa kwa kipindi cha mwaka mzima.

Hayo yamebainishwa leo Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mh Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mh Hawa Mchafu Chakoma aliyehoji serikali ina mpango gani wa kurasimisha vitambulisho vya wajasiriamali wadogo

Mh Dugange amesema kuwa tangu serikali ilipoanza utaratibu wa kuwapatia wajasiriamali vitambulisho imekuwa ikiendelea kufanya maboresho katika kuhakikisha inatatua changamoto za wajasiriamali hao.

Kwa upande mwengine Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema mfumo wa ulipaji Kodi ya Majengo kwa kutumia Mita za LUKU hautawahusu wapangaji, bali ni wamiliki wa nyumba husika

Akielezea suala hilo ametolea mfano mpangaji anapokuwa amelipa malipo ya mmiliki huwa anawasiliana na mwenye nyumba wake ili arudishiwe fedha yake.

Sanjari na hayo Wabunge 361 ambao sawa na asilimia 94 ya Bunge la Tanzania wameipiga Kura ya Ndio Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2021/22 ambapo Serikali imependekeza bajeti ya Tsh. Trilioni 36.26