Dodoma FM

Waziri wa mawasiliano awataka watoa huduma za mawasiliano kuboresha huduma zao

7 June 2021, 1:02 pm

Na; Shani Nicolous.

Waziri wa mawasiliano na teknolojia ya habari Dkt.Faustine Ndugulile amewataka watoa huduma za mawasilian nchini kuboresha huduma zao na kudhibiti laini zote zilizosajiliwa kimakosa.

Amesema hayo wakati akizungumza na watoa huduma za mawasilino nchini katika kikao kilichofanyika leo jijini hapa na kuahidi ushirikiano baina ya Wizara na watoa huduma hao .

Amesema kuwa Wizara iko mbioni kutangaza zabuni ya awamu ya sita ambayo imejikita katika kuboresha huduma za mitandao mipakani pamoja na Wilaya ambazo bado zinachangamoto ya mtandao.

Ameongeza kuwa wizara inatambua changamoto ya upatikanaji wa vibali kwa watoa huduma hao hivyo watajitahidi kurahisisha utoaji kwa wakati ili kutoa nafasi ya watoa huduma kuwekeza kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wao wadau wa mawasiliano nchini wameipongeza Wizara kwa mipango mizuri huku wakiahidi kushirikiana na Serikali kuboresha huduma hizo pamoja na kuongeza pato la Taifa kama zilivyo ndoto za Serikali.
Wameahidi kupunguza kero zitokanazo na mitandao kama utapeli na kufanya Watanzania kufurahia mawasiliano na mtandao bora na wenye tija kwa maendeleo.

Kikao hicho kimefanyika leo jijini Dodoma ambacho kimelenga kuwekana sawa baina ya wizara na watoa huduma za mawasiliano kwa ajili ya kutangaza zabuni za uwekezaji wa mawasiliano mipakani na wilaya zote ambazo bado zina changamoto ya mtandao.