Dodoma FM

Wananchi wa eneo la stendi kuu jijini Dodoma wameomba Serikali kuwawekea alama za barabara ( vivuko)

4 June 2021, 1:53 pm

Na, Victor Chigwada.

Wananchi wanaotumia kituo kikuu cha mabasi Dodoma pamoja na Soko kuu la Job Ndugai wameiomba Serikali kuwawekea kivuko cha juu pamoja na alama za barabarani kwenye eneo hilo ili kuepusha ajali.

Wakizungumza na Dododma Fm baadhi ya wananchi hao wamesema wingi wa watu wanaoelekea sokoni na kituo cha mabasi umekuwa ukiongeza hatari ya kupata ajali wakati wakivuka barabara kuu inayoelekea Morogoro na Dar es salaam.

Mwenyekiti wa mtaa wa Nzuguni A Bw.Onaely Mbatiani ameiomba mamlaka husika ikiwemo TANROAD kuweka kivuko ambacho wananchi watapita juu na magari kupita chini kwa ajili ya usalama zaidi.

Naye Diwani wa Kata ya Nzuguni Bw.Aloyce Luhega amesema kutokana na ukubwa wa barabara ni vyema kutengenezewa kivuko ili kuepusha ajali kutokana na idadi kubwa ya watu wanaovuka kuelekea kwenye kituo cha mabasi na sokoni.

Ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi na Soko kuu ni moja ya miradi mikubwa iliyotekelezwa jijini Dodoma ambapo tayari miradi hiyo imeanza kutumika huku ikiambatana na changamoto ndogondogo.