Dodoma FM

Jiji la Dodoma laagizwa kupanda miti katika maeneo yake yote

1 June 2021, 10:29 am

Na; Mariam Matundu.

Waziri mkuu wa Jmuhuri ya muungano wa Tanzania Mh.Kassimu Majaliwa ameliagiza jiji la Dodoma kuweka mpango mkakati wa maeneo yaliyopimwa na yanayopimwa kupandwa miti ili kuifanya Dodoma kuwa ya kijani .

Waziri mkuu ametoa kauli hiyo wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya mazingira leo jijini Dodoma ambapo amesema jiji la Dodoma linapaswa kubadilishwa na kuwa mfano wa kuigwa kwa mikoa yote ya Tanzania katika kutunza mazingira.

Amesema Dodoma inakabiliwa na changamoto nyingi za kimazingira ambapo ripoti ya 3 ya hali ya mazingira nchini ya mwaka 2019 inaonesha mkoa huo unakabiliwa na ukame na una kasi kubwa ya ukataji wa miti kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo matumizi ya kuni na mkaa.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais muungano na mazingira Mh.Selemani Jafo amesema wanatarajia kuzindua kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira mnamo tarehe 5 mwezi huu kampeni ambayo itahakikisha Tanzania inakuwa nchi ya mfano katika kutunza mazingira.

Mmoja wa wadau wa mazingira jijini hapa wanaozalisha mkaa mweupe John Lyadunda amesema ni wakati sasa serikali kuweka kanuni za kuzuia ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa ili jamii iachane na uharibifu wa mazingira na badala yake kutumia nishati mbadala.

Wiki ya mazingira imezinduliwa leo ambapo kilele cha maadhimisho hayo ni Juni 5 mwaka huu maadhimisho ambayo kitaifa yanafanyika jijini Dodoma yakiwa na kaulimbiu TUTUMIE NISHATI MBADALA KUOKOA IKOLOJIA.