Dodoma FM

Serikali kuboresha Mifumo ya upatikanaji wa Pembejeo

26 May 2021, 1:07 pm

Na; Yussuph Hans

Serikali Nchini inaendelea kuboresha Mifumo ya upatikanaji wa Pembejeo ikiwemo Mbegu, Mbolea na Viuatilifu, kuratibu katika Mikoa pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya makampuni kuuza maeneo mbalimbali.

Hayo yamebainishwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo Mh Hussein Bashe wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mh Stella Fiyao aliyehoji lini Serikali itapeleka pembejeo za kilimo kwa bei nafuu katika Mkoa wa Songwe ambapo wakulima wengi watamudu gharama hizo.

Mh Bashe amesema kuwa Serikali inaendela kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza upatikanaji wa pembejeo Nchini hasa mbegu, kwa kuvutia kampuni binafsi na mikataba maalumu ya uwekezaji.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo lililohoji kuhusu mkakati wa serikali kuleta mbegu bora ya alizeti kufuata uhaba wa mafuta hayo, Mh Bashe amesema kuwa kulingana na bajeti ya mwaka huu Serikali itahakikisha inazalisha mbegu za kutosha na bei nafuu kwa Wakulima.

Kwa upande mwengine Naibu wa Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh David Silinde wakati akijibu swali la Mbunge wa Chemba Mh Muhammed Lujuo aliyeuliza lini serikali itajenga barabara ya kwa mtoro kuelekea sanzawa mpaka mpendo kwa kiwango cha kupitika msimu mzima.

Mh Silinde amesema kuwa katika kipindi kwa mwaka fedha 2020/21 tarura wilaya ya chemba imetenga kiasi cha Mil 84.04 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo.

Bunge limeendelea leo Jijini Dodoma ambapo Wizara mbalimbali zimekwisha wasilisha Bajeti zake na Jana Bajeti ya Wizara ya Kilimo imewasilisha kwa mwaka wa fedha 2021/22.