Dodoma FM

Maji safi na salama changamoto kata ya mkonze

26 May 2021, 12:45 pm

Na; Mindi Joseph

Wakazi wa  mtaa wa Zinje Kata ya Mkonze jijini Dodoma wameiomba Serikali kuwapelekea maji safi na salama ili kuokoa afya zao kutokana na kutumia maji wanayochimba kwenye korongo ambayo si safi na salama.

Taswira ya habari imezungumza na wakazi hao ambapo wamebainisha kuwa maji ni uhai lakini hadi sasa Mtaa huo licha ya kuchimbiwa kisima kimoja lakini bado hakifanyi kazi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Zinje Bw.Gladife Daudi Samweli amesema licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali za kuchimba visima lakini havifanyi kazi hivyo ufuatiliaji wa makini unahitajika.

Wakati Mtaa wa Zinje ukikabiliwa na changamoto hiyo Tayari Jumla  ya Shilingi bilioni tano zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kutatua na kupunguza adha ya maji katika Mkoa wa Dodoma Fedha ambazo zinatumika  kuboresha miundombinu ya maji, ambapo hadi sasa  tayari visima 10, vimechimbwa vitatu kati ya hivyo vikiwa ni vikubwa na kimoja kitakua na uwezo wa kuchukua lita laki nne kwa saa.