Dodoma FM

Swaswa watakiwa kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wa umeme

21 May 2021, 10:21 am

Na; Benard Filbert

Wakazi wa mtaa wa Swaswa Kata ya Ipagala jijini Dodoma wametakiwa kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wa umeme ambao wamekuwa wakiweka nguzo kwa ajili ya usambazaji umeme wa REA awamu ya tatu.

Hayo yemesemwa na mwenyekiti wa mtaa huo Bw.Charles Nyuma wakati akizungumza na taswira ya habari juu ya zoezi ambalo limeanza hivi karibuni la uwekaji wa nguzo za umeme wa REA.

Amesema mtaa wa Swaswa ni miongoni mwa mitaa ambayo ipo kwenye mpango wa kuunganishiwa umeme wa REA awamu ya tatu hivyo kila mwananchi anatakiwa kuchangamkia fursa hiyo ipasavyo.

Amesema umeme huo utawasaidia kwa kiasi kikubwa ambapo hivi karibuni  wananchi watatangaziwa kuchukua fomu kwa ajili ya kuunganishiwa huduma hiyo.

Baadhi ya wakazi wa mtaa huo wamesema ujio wa nishati ya umeme katika eneo hilo ni fursa kwao kwa kuwa utawasaidia kwa kiasi kikubwa kujikwamua kiuchumi.

Swaswa ni miongoni mwa mitaa ambayo itanufaika na mradi wa umeme wa REA ambapo hivi karibuni wananchi wataanza kuunganishiwa.